Part 1..Finality of Prophethood by Maudodi

Mwisho wa Utume

S. Abul A’la Maududi

Anti Ahmadiyya Movement in Islam Utangulizi

Katika fitina zote zilizofanywa dhidi ya Uislamu katika zama hizi, fitina ya hatari

zaidi ni ile ya dai la Utume lililotolewa mwanzoni mwa karne hii.

Uzushi huu ukawa chanzo kikuu cha mcha*****o wa kiakili uliosambaa huku na kule miyongoni mwa Umma wa Waislamu kwa kipindi cha zaidi ya miyaka sitini iliyopita.

Kama vilivyo vyanzo vingine vya khitilafu, mzizi wa fitina hii ni kwamba Waislamu kwa ujumla ni mbumbumbu wa dini yao. Laiti wangelijitosha kwa elimu sahihi na kuushajiisha ufahamu sahihi wa nguzo ya imani ihusianayo na mwisho wa Utume, ingelikuwa vigumu mno kwa mzushi yeyote anaedai Utume kuotesha mizizi yake na kujistawisha miyongoni mwa Waislamu baada ya kipindi cha Mtume Muhammad (s.a.w).

Kwa nukta hii, tiba kamili na ya kufaa kuondosha uovu huu ni kuielimisha, kwa namna bora iwezekanayo, idadi kubwa ya watu juu ya Imani sahihi ya mwisho wa Utume wa Muhammad na kuusisitiza uzito na umuhimu wa kipengele hiki cha imani katika dini ya Uislamu.

Aidha ni shurti kwamba shaka zote na dhana zenye hatihati kuhusu kipindi cha mwisho cha Mtume Muhammad (s.a.w) ziondoshwe kwa hoja na mantiki. Kitabu hiki kimeandikwa ili kutimiza lengo hili.

Wasomaji wanaoyaona manufaa ya kitabu hiki hawana budi kupiga hatuwa mbele kutowa ushirikiano wao katika kusambaza maudhui yake. Yapasa kitabu hiki kiwafikiye watu wote wanaojuwa kusoma na baada ya wao wenyewe kukisoma wawasomee wasiojuwa kusoma.

Yatumainiwa kuwa usomaji wa kitabu hiki siyo tu utawakinga wale ambao hawajasibiwa na gonjwa hili bali piya utauweka bayana ukweli kwa watu wenye akili nzuri ya kufikiri miongoni mwa wale waliopata vimeleya vya maradhi.

Hata hivyo wale ambao wamekuwa wahanga wa uzushi na wasiosikiya nasaha, basi, kwao wao, tumaini na nusura ipo kwa Allah pekee.

Abul A’la Maududi

Lahore

Februari 12, 1962.

Kwa jina la MwenyeziMungu Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu

Mwisho wa Utume

“Muhammad si baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, bali yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Mitume. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu”. (33: 40)

Aya hii imefunuliwa katika Rakaa ya tano ya surati Ahzab. katika Rakaa hii MwenyeziMungu ametowa majibu ya hoja zote zilizotolewa na wanafiki, ambazo zilikuwa zimezusha kimbunga cha minong’ono, kashfa na fitina kuhusiyana na ndowa ya Mtume Muhammad (s.a.w) na bi Zainab (r.a).

Wanafiki hawa walidai kuwa Zainab alikuwa mke wa mtoto wa kupanga wa Mtume Mtukufu na kwa uhusiyano huu bibi huyo alisimama mahala pa mkwe wa Mtume. Ndiyo kusema baada ya kutalikiwa na Zaid, Mtume alimuowa mkwewe.

Ili kulikanusha dai hili MwenyeziMungu akasema waziwazi katika aya ya 37 kuwa ndowa hiyo nyuma yake ilikuwa na sheriya ya Mungu na ilifanywa hivyo ili itumike kama ruhusa ya kisheriya kwa Waislamu wanaume kuwaowa wake wa watoto wao wa kupanga baada ya kutalikiwa na waume zao.

Baadaye katika aya ya 38 na 39, Mwenyezi Mungu akamueleza Mtume kwamba hakuna mamlaka ya kumzuwiya Mtume kutekeleza hukumu ya Mwenyezi mungu. Mitume wanaamrishwa kumchelea Mungu tu na si watu.

Hiyo ndiyo ada isiyobadilika ya Mitume kueneza ujumbe wa MwenyeziMungu pasina kujali hali yoyote ya nje na kutekeleza majukumu waliyopewa na MwenyeziMungu bila hofu wala kusitasita.

Baadae ndipo ikashushwa aya ambayo ilivunjiliya mbali msingi wa hoja zote. Kwanza walimshutumu, “Umemuwowa mkweo, ukipingana na sheriya yako mwenyewe kuwa mke wa mtoto ni maharimu kwa babaye”.

Katika kujibu shutuma hii ndipo ikasemwa na Mwenyezi mungu; “Muhammad si baba wa yoyote kati ya wanaume wenu ..”

Hapo ikawekwa bayana kabisa kuwa yule mtu ambaye mke aliyetalikiyana nae aliolewa na Mtume si mtoto wake halisi; kwa hiyo jambo hilo halikuwa na maana ya kukiuka sheriya.

Hoja ya shutuma yao ya pili ilisema “ Sawa ikubalike kuwa mtoto wa kupanga si mwana halisi, na kwa msingi huo, huwenda baba angeweza kisheriya kumuowa mtalaka wa mtoto wake wa kupanga, lakini kulikuwa na ulazima gani kwa Mtume kufanya hivyo?

Katika kujibu shutuma hiyo Allah akasema:

“Lakini kwa hakika yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu “ Maana yake ni kwamba hiyo ilikuwa ni amri ya MwenyeziMungu kwa Mtume kufutiliya mbali kasumba zote na kuondoshi ile miiko ambayo mila ya kipagani, pasina ulazima wowote, iliwawekeya watu. Kwa ajili hii, hatuwa ya Mtume ilikuwa ni sahihi na hapakuwa na sababu tena ya kuitiliya shaka.(Taz. Tanbihi 1 chini).

Ili kuiwekeya msisitizo mahususi nukta hii, MwenyeziMungu anasema; (Khatim Al-Nabiyiin) “Naye ndiye Mwisho wa Mitume”

Ambayo ina maana kuwa baada ya Muhammad, hakuna Mtume wala Nabii atakayekuja kufanya mambo mengine ya kisheriya na ya kijamii ambayo labda ( SubhanAllah) yangekuwa yameachwa wakati wa Muhammad.

Kwa vile Mwenyezi Mungu aliamuwa kipindi cha Mtume Muhammad kiwe cha mwisho, , basi, ilibidi yeye akamilishe kazi ya kung’owa mizizi ya mila hii ya kipagani.

Baadae jambo hili likasisitizwa zaidi katika wahayi (Wa Kan ul- Allahi Bi-kulli Shai-in Aliima): “Na MwenyeziMungu ni Mjuzi wa kila kitu”

Maana sahihi ya wahai huu ni kwamba MwenyeziMungu aliona ni heri zaidi kuindosha mila hii ya kipagani kupitiya utume wa Nabii Muhammad na kwamba Yeye MwenyeziMungu aliyajuwa madhara ambayo mila hii ya kikafiri ingeyaleta kama ingeendeleya.

MwenyeziMungu alikwishajuwa fika kuwa mlolongo wa Utume uliishiya kwa Muhammad ambaye kigezo chake kitafuatwa na Umma mzima, ambapo kama asingeiondosha mila hii basi pasingelitokeya tena mtu mwenye daraja sawa na la Mtume Muhammad ambaye angekamilisha kazi hiyo.

Jaaliya hata kama angetokeya Mujaddid baada yake na kuvunja mila hii, hatuwa yake isingeliweka kigezo cha ulimwengu mzima na cha kudumu kwa Waislamu wa zama zote na nchi zote kukifuwata.

Hakuna mtu mwingine wa kuja baada yake ambaye atapambika kwa utakaso wa Mungu unaolingana na wasifu wa Muhammad. Ndiyo kusema ukimuondowa Muhammad hakuna kigezo cha mtu mwingine kinachoweza kufutiliya mbali kasumba ya mila za kipagani katika nafsi za watu wa zama zote.

Hukumu ya Aya ya Qur’an

Kundi ambalo limeeneza uzushi wa Utume mpya katika zama hizi, linafafanuwa maana ya dhana ya “Mwisho wa Utume” kuwa ni muhuri wa Unabii, hii ikiwa na maana kuwa Mitume wote watakaokuja baada ya Muhammad (s.a. ) watabandikwa Muhuri huu, na watapata Utume kwa muhuri wake tu. Kwa maneno mengine, yule ambaye habandikwi muhuri wa Muhammad hatapata daraja la Utume.

Lakini muktadha ambamo kauli hii “Yeye ni wa Mwisho wa Mitume” imeshushwa katika Qur’an tukufu hauwachi upenyo wa kupenyezeya uzushi huo. Kama kweli kauli hii ya “mwisho wa Mitume” ina maana inayokusudiwa na kundi hili, basi kwa hakika kauli hii inatolewa nje ya muktadha ambamo imefunuliwa. Isitoshe, pindi kauli hii inapopewa maana hii basi inavuruga kusudio zima la aya husika.

Katika aya hii Mwenyezi Mungu (s.w) anakanusha shutuma na kuondosha shaka zilizoletwa na Mafatani kuhusiyana na ndowa ya Mtume Muhammad na bibi Zainab, mtalaka wa Bwana Zaid ambaye ni mtoto wa kupanga wa Mtume (s.a.w).

Je inaleta mantiki kuugeuza ghafla muktadha wa kauli hii kwamba eti Muhammad alikuwa ‘muhuri wa Mitume’ na kwamba eti MwenyeziMungu alikuwa amemuweka Muhammad katika mamlaka ya kuthibitisha ukweli wa Mitume wajao?

Tafsiri hii haina mnasaba na muktadha hata kidogo na inakwenda kinyume na kusudio la hoja ya Mungu dhidi ya wazushi. Kama tafsiri hii ingekuwa sahihi basi Makafiri wangeliweza kutowa hoja nzuri kabisa (kwa kumwambiya Muhammad kuwa):

“Hakuna haja ya kuharakisha kuindowa mila hii kwa sasa. Unaweza kuiacha kazi hii kwa Mitume watakaokuja baada yako ambao watabandikwa Muhuri wako.”

Kwa mujibu wa tafsiri ya pili ya dhana ya mwisho wa utume iliyovumishwa na kundi hili inasemwa kuwa eti kauli hii, “Mwisho wa Mitume” maana yake ni “Mtume aliyetukuzwa”.

Wanafafanuwa zaidi kuwa mlolongo wa Mitume utaendeleya, ingawaje utukufu wa Mitume umekomeya katika wasifu wa Muhammad. Tafsiri hii haina uharibifu mdogo na ina madhara zaidi kuliko hata ile nyingine.

Haina mnasaba kabisa na muktadha na, kwa kweli, inaleta maana inayopingana na aya. Kwa kutumia upenyo wa hoja hii, Makafiri na wanafiki, kwa kutafuta kisingizio, wangesema,

“Bwana, si kutakuwa na Mitume wengine wa kukamilisha kazi ya Mungu baada yako’ ingawaje wana daraja la chini kulinganisha na wewe, kwa nini basi ulazimike wewe tu kuindosha mila hii?”

Maana Neno khataman Nabiyyin katika kamusi:

Ni Dhahiri kuwa aya tuliyoinukuu ina maana moja tu nayo ni kuwa khaataman Nabiyyin ni mwisho wa Utume ikiwa na maana kuwa utume umekoma na umekamilishwa na Muhammad. Siyo tu muktadha wa aya bali hata kamusi inaunga mkono tafsiri hiyo.

Kwa mujibu wa kamusi ya Kiarabu sanifu na kwa mujibu wa matumizi ya kilugha, Khaatam maana yake ni kupiga muhuri kufunga, kufikia mwisho na kukifikisha kitu fulani katika hatima yake.

Khatama al’ Amala ni sawa na “Faragha min al Amali” yenye maana ya kukamilisha jukumu. “Khatama al-Ina” inabeba maana kuwa chombo kimefungwa kiasi ambacho hakuna tena kitu kinachweza kingia ndani yake, wala vile vilivyomo haviwezi kumwagika nje”.

“Khatam-al-Kitab” lina maana kwamba Baruwa imefungwa na kupigwa muhuri au rakili ili ibakiye salama hadi mwisho.

“Khatama-Ala-al-Qalb” lina maana kwamba moyo umefungwa kiasi kwamba hauwezi kufahamu chochote kipya wala hauwezi kuachana na kile ambacho kimo ndani yake.

‘Khitamu-kulli –Mashrubin’ lina maana ya ladha inayobakiya mdomoni pale kinywaji kinapokwisha.

Katimatu Kulli Shaiinn Aqibatuhu wa Akhiratuhu lina maana kwamba mwisho wa kila jambo ndio unaoashiriya maangamizi na hatima yake. Khatm-ul-Shaii Balagha Akhirahu linabeba maana ya kulimaliza jambo kwa maana ya kulifikisha mwisho wake.

Neno Khatam-i-Qur’an hutumika kwa maana hiyo hiyo ambapo aya za mwisho za sura za Qur’an huitwa Khawatim. Khatim-ul-Qaum Akhirhuun: maana yake ni “mtu wa mwisho katika ukoo”.(Taz. Lisan-ul-Arab; Qamus na Aqrab-ul-Muwarid). (Taz. Tanbihi 2, chini)

Kwa maana hizi, Mabingwa wa Lugha na Mufasiruna wote wanakubaliana kuwa Khatam-ul-Nabiyyin maana yake ni “Wa mwisho katika mlolongo wa Mitume.”

Neno Khatam kwa maana yake ya kamusi na kwa matumizi yake ya kilugha halihusiyani na muhuri wa Posta unaopigwa juu ya bahasha ya baruwa inayotumwa. Maana yake ya kiistilahi ni lakiri ambayo huwa nje ya bahasha ili kuhakikisha usalama wa vile vilivyomo ndani yake.

Maneno ya Mtume yathibishayo mwisho wa utume

Maana ya neno Khaatam ambayo inajitokeza katika muktadha wa Qur’an na ambayo ni sawa na ile iliyotolewa na kamusi zote za lugha ya kiarabu piya inashadidiwa na maneno ya Mtume Mtukufu (s.a.w). Hapa tunanukuu baadhi ya Hadithi sahihi kusherehesha maana hiyo.

Mtume mtukufu wa Allah amesema “Bani Israil waliongozwa na Mitume, pale alipotawafu Mtume mmoja, alikuja mwingine. Lakini hakuna Mtume atakayekuja baada yangu. Ni Makhalifa tu watakaokuja baada yangu” (Bukhari kitabul Manaqib).

Pia amesema “nafasi yangu kuhusiyana na Mitume waliokuja kabla yangu inaweza kufafanuliwa kwa mfano huu; Mtu amejenga jengo na kuliremba kwa nakshi nzuri, lakini pembeni mwa jengo hilo ameacha uwazi ambao tofali moja tu limekosekana.

Watu wakalitazama jengo hilo na kulistaajabiya uzuri wake, lakini wakashangazwa kwa nini tofali moja limekosekana kwenye uwazi huo? Basi mimi ni mfano wa hilo tofali lililokosekana kwenye uwazi huo na hivyo mimi ni wa mwisho kabisa katika mlolongo wa Mitume. (Bukhari kitab- ul -Manaqib)

Kwa maneno mengine, kwa kule kuja kwa Mtume Muhammad (saw) jengo la Utume limekamilika na hivyo hakuna tena uwazi katika jengo hilo kwa ajili ya Mtume mwingine.

Takribani hadithi nne zinazohusu jambo hili zimo katika Muslimu, kitab ul Fada’il, Bab-ul-Khatmin-Nabiyyin. Hadithi ya mwisho ina kauli hii ya nyongeza; “Kwa hivyo, Mimi ndiyo nimekuja na ni kwangu mimi ndipo ulipoishiya ule mlolongo wa Mitume.”

Hadithi kama hiyo vile vile imeripotiwa kwa maneno hayo hayo katika Tirmidhi, kitab ul Manaqib, Bab Fadlin Nabi na Kitab Adab, Bab ul Amthali. Na katika Musnad Abu Dawud Tayalisi Hadithi hii imejumuishwa na hadithi nyingine zilizoripotiwa na Jabir bin Abdullah ambapo kauli ya mwisho ni hii; ni “kwangu mimi ule mlolongo wa Mitume umefika kikomo chake”.

Musnad Ahmad nayo ina Hadithi zilizoripotiwa na Ubayyi bin Ka’b, Abu said Khudri na Abu Huraira (Alla awawie radhi) ambazo zote zinahusu kauli Hiyo hiyo ukiyacha tofauti ndogo tu ya maneno hapa na pale.

Vile vile Mtume wa Allah amesema: “MwenyeziMungu amenineemesha neema sita ambazo Mitume waliotanguliya hawakuwa nazo:

-Nimejaaliwa neema ya kusema kwa kauli fupi zenye maana kamili.

-Nilipewa ushindi kutokana na unyenyekevu wangu wa hofu.

-Vilivyotekwa vitani vilihalalishwa kwangu

-Ardhi yote kwangu imefanywa mahala pa kufanyiya ibada na piya imekuwa sehemu ya kujitwaharishiya kwangu. Kwa maneno mengine katika dini yangu kuswali hakukomei katika sehemu mahususi za ibada. Sala yaweza kusaliwa mahala popote ardhini. Na endapo maji hayapatikani inaswihi watu kufanya tayamumi na kujitwaharisha kwa udongo iwapo maji ya kuogeya ni haba.

-Nimetumwa na Allah kueneza ujumbe wake ulimwenguni kote

- “Mlolongo wa Mitume umeishia kwangu” (taz. Muslimu Tirmidh na Ibn Majah.)

Akasisitiza Mtume wa Allah, “Mnyororo wa Mitume na Manabii umefikiya ukomo. Hakutakuwa na Mtume wala Nabii baada yangu. (Tirmidh, Kitab-ur-Rouya Babu Zahab-un- Nubuwwa, Musnad Ahmad, Marwiyat-Anas bin Malik).

Zaidi ya hivyo, Mtume wa Allah amesema “Mimi ni Muhammad na mimi ndio Ahmad, mimi ni kifutiyo na kufuru itafutwa kupitiya kwangu. Mimi ni mkusanyaji na watu watakusanywa siku ya hukumu baada ya kipindi changu. Nami ndiye wa mwisho kwa maana hakuna tena Mtume atayekuja baada yangu.( Kwa maneno mengine hukumu ndiyo itakayokuja baada yangu).

(Bukhari na Muslim, Kitab-ul-Fada’il. Bab: Asmaun-Nabi; Tirmidhi, Kitab-ul, Adab, bab: Asma-un-Nabi: Muatta” Kitab-u-Asma in-Nabi, Al-Mustadrak Hakim, Kitab-ut -Tarikh, Bab: Asma-un-Nabi).

Mtume (s.a.w) ameongeza kusema, “Mwenyezi Mungu Hakutuma Mtume yeyote ulimwenguni ambaye hakuwahadharisha watu wake juu ya kuja kwa Dajjal (lakini Dajjal hakutokeya katika zama zao). Mimi ni wa mwisho katika mlolongo wa Mitume na nyie ndio umma wa mwisho wa walioamini, basi bila shaka Dajjal atatokeya miyongoni mwenu”. (Taz. ibn majah, kitabul- Fitan, Bab: Dajjal).

Bwana Abdul Rahman bin Jubeir naye ameripoti; “nilimsikiya Abdullah bin “Amr ibn ‘As akisimuliya kuwa siku moja Mtume mtukufu alitoka nje ya nyumba yake na kukaa pamoja nasi. mazungumzo yake yalitoa taswira kana kwamba alikuwa anaagana nasi, alisema “Mimi ni Muhammad, Nabii asiyejuwa kusoma wala kuandika “ na akarudiya kauli hii mara tatu, kisha akasema, “hakutakuwa na Mtume baada yangu “ (Taz. Musnad Ahmad, Marwiyat’ Abdullah bin Amri ibn’ As).

Mtume mtukufu kasema: “Allah hatatuma Mtume baada yangu, isipokuwa Mubashshirati. Ikaulizwa nini maana ya Mubashshirat. Akasema ndoto njema, au ndoto ya uchaMungu” (Musnad Ahmad, Narwiyat Abu Tufail. Nasa’i, Abu Dawud).

( Kwa maneno mengine hakuna uwezekano wa kuja wahai kutoka kwa Allah, sanasana kama mtu anapata ilhamu basi ataipata kwa njia ya ndoto njema).

-Mtume mtukufu (saw) amesema: “Kama angelikuja Mtume baada yangu basi angelikuwa “Umar bi Khattab”. ( Tirmidhi, Kitab-ul-Manaqib).

-Mtume Mtukufu alimwambia Ali, “wewe unanasibiyana nami kama Harun alivyonasibiyana na Musa (as). Lakini hakuna Mtume atakayekuja baada yangu “ (Bukhari na Muslim, Kitab Fada’il as-sahaba).

Hadith hii piya imenakiliwa ndani ya Bukhari na Muslim katika maelezo ya Vita ya Tabuk.

Musnad imenakili Hadithi mbili zilizosimuliwa na Sa’d bin Abi Waqqas (ra) ambazo zote zinahusu jambo hili. Kauli ya mwisho katika moja ya Hadith hizi inasomeka hivi: “sikilizeni hakuna Unabii baada yangu”.

Maelezo ya kina ya Hadithi zilizokusanywa katika Abu Dawud Tayalisi, Imam Ahmad na Muhammmad bin Ishaque yanasema kuwa, kabla ya safari yake ya kwenda vitani katika vita ya Tabuk, Mtume mtukufu alikuwa amepanga kumuwacha nyuma Sayidina Ali ili achunge ulinzi na kusimamiya shughuli za madina.

Hapo wanafiki wakaanza kusambaza vijineno vya chini chini na uzushi kuhusu Sayidina Ali. Sayidina Ali akaenda kwa Mtume na kusema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu unaniacha mimi nyuma nibaki na wanawake na watoto?” Hapa ili kutuliza fikra zake Mtume akasema: “wewe unahusiyana nami kama alivyokuwa Harun na Musa.”

Kwa maneno mengine “kama vile Musa alivyokwenda mlima Tua na kumwacha Harun nyuma awachunge wana wa Israili ndivyo mimi ninavyokuwacha wewe nyuma kuchunga ulinzi wa Madina.” Lakini wakati huo huo, kwa kufahamu kuwa mfano huu wa kujilinganisha na Ali ungeliweza kusababisha uzushi baadaye, Mtume (saw) palepale akaweka wazi kuwa “Hakutakuwa na Mtume baada yangu”.

Thauban ameripoti: “Mtume mtukufu (saw) alisema:“ Watakuja kutokeya wazushi thelathini katika umma wangu ambapo kila mmoja kati yao atautangaziya ulimwengu kuwa yeye ni Mtume, lakini Mimi ndiye wa mwisho katika mlolongo wa Mitume wa MwenyeziMungu ambapo hakuna Mtume atakayekuja baada yangu” (Abu Dawud, Kitab-ul-Fitan).

Abu Dawud katika “Kitab-ul-Malahim” amenakili Hadith nyingine iliyoripotiwa na Abu Huraira kuhusiana na jambo hilo hilo. Tirmidhi piya amenakili Hadith hizi mbili kama zilivyoripotiwa na Sayidina Thauban na Abu Huraira. Maneno ya Hadith ya pili yanasema hivi: “Itakuja kufikiya hivi kuwa wazushi thelathini watazuka na kila mmoja atatangaza dai lake kuwa yeye ni Mtume wa Mungu.”

-Mtume Mtukufu amesema: Miongoni mwa bani Israili waliopita kabla yenu, kwa hakika, kulikuwa na watu waliokuwa na mawasiliano na Mungu, hata hivyo hawakuwa Mitume wake. Kama pangetokea mtu miongoni mwa watu wangu ambaye angekuwa na mawasiliyano na Mungu, basi asingekuwa mwingine ila Umar (r.a) (Bukhari, Kitab-ul-Manaqib).

Tafsiri ya Hadith hiyo hiyo katika ‘Muslim’ ina Muhaddithuna badala ya Yukallimuna. Lakini hapo Mukalima na Muhaddith yote yanabeba maana ile ile.. yaani mtu apataye fursa ya kufanya mawasiliano ya moja kwa moja na MwenyeziMungu au mtu anayesemeshwa na Mungu kutoka ughaibuni. Hivyo tunahitimisha kuwa kama kungelikuwa na mtu yeyote miongoni mwa wafuwasi wa Muhammad ambaye angekuwa na mawasiliyano na Mungu bila kupandishwa katika daraja la Utume, basi angekuwa Umar.

-Mtume wa Allah kasema: “Hakuna Mtume atakayekuja baada yangu, na ndio kusema, hakutakuwa na umma mwingine wa wafuwasi wa Mtume yeyote mpya”. (Baihaqi, Kitab-ul Rouya: Tabarani)

Mtume Mtukufu kasema: “Mimi ndiye wa Mwisho katika mlolongo wa Mitume wa Mungu na Msikiti wangu ndio Msikiti wa mwisho (hii ikiwa na maana ya Msikiti mtukufu wa Mtume) (Taz.Tanbihi 3) (Muslim, Kitab-ul-Hajj; Bab: Fadiu-us-Salat bi Masjidi Maka wal Madina)

Idadi kuwa ya Hadith kama hizo za Mtume mtukufu (s.a.w) zimeripotiwa na Maswahaba na Wakusanyaji wengi mashuhuri wamezinakili kutoka katika vyanzo sahihi.

Utafiti wa Hadith hizi unaonesha kuwa, Mtume mtukufu, mara kadhaa, na kwa njia mbali mbali na kwa maneno tofauti alibainisha wazi kuwa yeye ni Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu; Kwamba hakuna Mtume atakayemfuatiya yeye na kwamba ule mlolongo wa Mitume umeishiya kwake. Hivyo basi, wale wote watakaodai kuwa ni Manabii na Mitume wa Mungu ni wazushi na warongo. (Taz.Tanbihi 4)

Hapawezi kuwa na tafsiri sahihi, ya kuaminika na ya hakika ya maneno ya Qur’an, Khatam-un-Nabiyyin, zaidi ya ile iliyotolewa na Mtume (saw) kwani maneno ya Mtume Mtukufu hayahitaji kuthibitishwa wala usahihi wa maneno yake hauwezi kuhojiwa. Maneno yake ndiyo sahihi na ndiyo uthibitisho wenyewe. Pale Mtume anapofafanua jambo fulani la Qur’an, ufafanuzi wake ndio sahihi na ndio uthibisho madhubuti.

Sasa swali ni hili, nani mwingine zaidi ya Mtume mtukufu (s.a.w) aliyefunuliwa Qur’an, ambaye anastahili zaidi kuielewa maana yake na kutowa ufafanuzi wa maudhui yake? Je yule anayetowa ufafanuzi mwingine badala ya ule wa Mtume tutayachukuliyaje madai yake kuwa yanaswihi hata kupewa mazingatiyo yetu achiliya mbali kuyakubali.

Shura ya Maswahaba

Baada ya Qur an na Sunna, Shura ya Maswahaba wa Mtume (s.a.w) ndiyo inayoshika nafasi ya tatu. Riwaya zote sahihi za kihistoriya zinabainisha kuwa Maswahaba wa Mtume wote, kwa pamoja, waliwapiga vita wale wote waliodai utume pamoja na wafuwasi wao baada ya kutawafu kwa Mtume mtukufu.

Kwa munasaba wa jambo hilo, kisa cha Musailama kina uzito mahususi. Si kwamba bwana huyu alikanusha kuwa Muhammad ni Mtume wa MwenyeziMungu; bali alidai kuwa Mungu alimteuwa yeye kuwa Mtume-mwenza wa Muhammad ashirikiyane naye kwa kazi hiyo. Baruwa ambayo ilitumwa kwa Mtume punde kabla ya kifo cha Musailama inasomeka hivi;

“Kutoka kwa Musailama Mtume wa Mungu kwenda kwa

Muhammad Mtume wa Allah. Napenda kukutaarifu kuwa

rnimeteuliwa kuwa Mshirika wako kushirikiyana nawe katika

jukumu la utume.” Mwanahistoriya mkubwa Twabari

amenukuu Hadith ambayo inasema kuwa (Musailama

alishuhudiya): “Nashuhudiya kuwa Muhammad ni Mtume wa

Mungu.”

Licha ya shahada ya Musailama kuhusu utume wa Muhammad, bado alitangazwa kuwa ni murtadi na akatengwa kabisa na jamii ya Waislamu. Si hivyo tu bali vita vikaanzishwa dhidi Musailama.

Historiya vilevile inauthibitisha ukweli huu kuwa kabila la Hunaifa(Banu Hunaif) lilikubaliana na dai la unabii la Musailama kwa imani ya dhati. Walidanganyika hata kuamini kikwelikweli kuwa Muhammad (s.a.w) kwa hiyari yake, amemtangaza Musailama kama nabii mwenza.

Mtu mmoja aliyesoma Qur an katika Mji Mtakatifu wa Madina aliwaendeya Banu Hunaif na kuwazuga kwa kuwapa aya za Qur an zilizodaiwa kushushwa kwa Musailama.

Ijapokuwa Banu Hunaifa walipotoshwa kwa makusudi, lakini Maswahaba wa Mtume Mtukufu hawakuwatambuwa watu hao kama Waislamu na Wakapeleka jeshi dhidi yao.

Hapa hakuna mwanya wa kupachika dhana kuwa Maswahaba walipambana na watu hao kama waasi na siyo Muratadi. Shariyah ya Kiislamu imeweka kanuni kuwa inapotokeya vita dhidi ya Waislamu walioasi, mateka wa vita hawatatiwa utumwani. sheriya inasisitiza kuwa hata waasi wasiyo Waislamu (Madhimi) wanapokamatwa mateka vitani, hawatatiwa utumwani.

Lakini pale hatuwa ya kijeshi ilipochukuliwa dhidi ya Musailama na wafuwasi wake, Sayidina Abubakar aliamuru kuwa wanawake na watoto wa aduwi wachukuliwe kama watumwa na pale walipokamatwa mateka walitiwa utumwani. Miyongoni mwao alikuwemo binti mmoja ambaye alitolewa kama suria wa Sayidina Ali.

Akamzaliya mtoto wa kiume aliyeitwa Muhammad bin Hanfiya ambaye ni mtu mashuhuri katika historiya ya Uislamu. (Al-badaya wan-Nahaya, juzuu ya 6, ukurasa 316-325)

Tukiyo hili ni uthibitisho wa wazi wa ukweli kuwa wakati Maswahaba walipombana na Musailama, hawakumuhukumu kwa uwasi. Hukumu dhidi yake ilikuwa kwamba yeye alijitangazia utume baada ya mlolongo wa Mitume kuishiya kwa Muhammad ambapo aliwapotosha watu wengine ambao walishikiliya imani juu ya dai lake la utume.

Hatuwa hiyo dhidi Musailama ilichukuliwa muda mfupi tu baada ya kutawafu kwa Mtume Mtukufu chini uwongozi wa Abubakar Sidiq (r.a) na ilikuwa imeungwa mkono na shura nzima ya Maswahaba. Hapawezi kupatikana kigezo bora na cha wazi zaidi cha shura ya maswahaba kama hiki.

Shura ya Maulamaa wote wa Umma

Ngazi inayofuwata baada ya Shura ya Maswahaba ni Shura ya Maulamaa miyongoni mwa Waislamu waliokuja baada ya kipindi cha maswahaba.

Jicho katika historiya nzima ya Uislamu kuanziya karne ya kwanza hadi zama hizi linatubainishiya ukweli kuwa Maulamaa wa zama zote katika kila nchi ya kiislamu ulimwenguni kote, kwa ujumla, wameshikiliya imani moja kuwa hakuna tena Mtume atakayekuja baada ya Muhammad (s.a.w).

Wote wanakubaliyana na hukumu kuwa mtu yeyote anayedai utume baada ya Muhammad na mtu yeyote anayesadiki dai la mtu huyo ni murtadi na atengwe kabisa na jamii ya kiislamu.

Matukiyo yafuatayo yanarejelewa kama viyelelezo:

· Enzi ya Imam Abu Hanifa yaani miyaka ya (80-150 Hijiriya), mtu mmoja alijitokeza kudai unabii ambapo alisema “ngojeni nikuonesheni dalili za unabii wangu” Imam, papohapo, akawaonya watu kwamba “Yeyote anayetaka dalili za unabii kutoka kwa mtu huyo naye atakuwa Murtad kwani Mtume wa Allah amekwishatangaza wazi kuwa “hakuna Nabii atakayekuja baada yangu”. (Taz. Manaqib al-Imam-i- Azam Abi Hanifa, Ibn Ahmad al Makki, juzuu ya 1 uk. 161, iliyochapishwa Hyderabad, India,1321 A.H).

· Katika tafsiri yake mshuhuri ya Qur an, Imam Ibn Jariri Twabari aliyeishi katika miyaka ya 224-310 Hijiriya, ametowa tafsiri ya aya isemayo “Walakin Rasul Allahi wa Khatam-ul Nabiyyin” kama ifuatavyo; ameufunga na kuukomea unabii na kwa hiyo mlango (wa unabii) hautafunguka tena kwa ajili ya mtu yeyote yule hadi mwisho wa duniya (Taz. Tafsiri Ibn-i-Jarir, juzuu ya 22, uk. 12).

· Katika kitabu chake Aqida –i- Salfiya, akielezeya imani za wachaMungu walioshikamana na subira hasa hasa imani za Maimamu Abu Hanifa, Imam Abu Yusuf, Imam Muhammad na Imam Tahawiy aliyeishi miyaka ya 230-321Hijiriya, ameandika kuwa Muhammad (s.a.w) ni mja wa Allah mwenye cheo cha juu kabisa cha utukufu. Yeye ni Mwisho wa Manabii. Kiongozi wa wacha Mungu, Mkuu wa Mitume wa Allah na mja mpendwa wa Mwenyezi Mungu. Baada yake yeye kudai utume ni dhambi iliyodhahiri na ni uovu wa kuabudiya nafsi. (Sharah al -Tahawiya Fil” –Aqidat-ul-Salfiya,Dar–ul-Ma’arif, Misri, Ukurasa wa 15,87,96,97,100,102.)

· Ulamaa Imam Ibn Hazm Andulasi aliyeishi miyaka ya 384-456 Hijiriya, naye ameandika hivi : “Ni jambo la hakika kuwa wahyi umefikiya ukomo baada ya kutawafu kwa Mtume mtukufu. Ushahidi wa hilo unategemeya ukweli kuwa hakuna yeyote anayeweza kupokeya wahyi wa Allah isipokuwa Mtume, na Allah ndiyo hivyo amethibitisha kuwa Muhammad si baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu bali yeye ni Mtume wa Allaha na amefunga ofisi ya unabii” (Al Muhala juzuu ya 1 ukurasa 26)

· Imam Ghazali aliyeishi miyaka ya 450 hadi 505 Hijiriya anasema iwapo haki ya kupinga hukumu ya shura itatolewa, itasababisha yazuke mambo mengi yasiyo na kichwa wala miguu. Mathalani, kama mtu akisema kuwa inawezekana kwa mtu kuipata tena ofisi ya Unabii baada Mtume wetu Muhammad (s.a.w), kweli, sisi hatutasita kumtangaza mtu huyo kuwa ni kafiri. Lakini katika malumbano, mtu anayetaka kuthibitisha kuwa upinzani wowote dhidi ya hukumu ya kumtambuwa mtu huyu kama Murtadi ni uwasi atalazimika kutafuta nguvu ya shura kuunga mkono hoja zake. Kwa sababu hoja pekee si suluhisho la kuzuiya uwezekano wa kuzuka “nabii mpya.” Kwani wafuwasi wa manabii wapya hawatashindwa kabisa kutowa tafsiri nyingine ya “La Nabiya Ba’di. Yaani “hakutakuwa na nabii baada yangu” na khatamul Nabiyyin- Mwisho wa Mitume. Mfuwasi wa Mitume wapya anaweza kusema kuwa Khatam-ul-Nabiyyin, Mwisho wa Mitume maana yake ni mwisho wa wale Mitume mashuhuri.” Na kama wewe ukitowa hoja kuwa “ Manabii ni neno la jumla, basi mtu huyo kirahisi kabisa ataipa istilahi hiyo uzito mahususi kwa mnasaba wa unabii wake.

Na kuhusu sentesi hii kuwa hakuna Nabii atakayekuja baada yangu,” mtu huyo anaweza kudai kuwa usemi huu hauna maana kuwa Hakuna Mitume watakaomfuwata”. Ipo tofauti kati ya Nabii na Mtume. Hadhi ya Nabii ni kubwa kuliko ile ya Mtume.

Kwa hiyo, ukweli ni kuwa madai ya kipuuzi kama hayo yanaweza kuwa mengi pasina kiyasi. Kwa mtazamo wetu huwo, si vigumu kutowa tafsiri tofauti za Istilahi hiyo.

Mbali na hivyo, Pamoja na kuwa hakuna upenyo kwa watu kutumbukiya makosani na kwenda kinyume katika kuyafasiri maneno haya yaliyowazi, bado hutuwezi kusema kuwa wale wanaotowa tafsiri za namna hiyo wana hatiya ya kupinga hukumu zilizo bayana .

Lakini ili kuwakana wale ambao wanaamini tafsiri hizo potofu kwa makusudi ya nafsi zao, tutalazimika kutamka hivi; kwamba umma kwa ujumla kupitiya shura ya rai, unayatambuwa maneno “hakuna Nabii atakayekuja baada yake” na muktadha wa hadith unabainisha kwamba “hakuna Nabii wala Mtume” atakamyefuata.

Isitoshe Umma, kwa ujumla, unakubaliyana na hoja kuwa maneno hayo ya Mtume mtukufu hayakuwacha mwanya wa kutoleya tafsiri ya aina nyingine inayotofautiana na hiyo ya shura ya Ummah na yule ambaye hataungana na shura basi ni mpizani ( Al-Iqtisad Fil Aitiqad uk. 114, Misri)

(Tumenukuu matini yenyewe ya Kiarabu(katika toleo la Kiudu) ya rai ya Imam Ghazali kwa sababu wakanushaji wa dhana ya Mwisho wa Utume wamepinga usahihi wa Rejeleo hili).

Mohyi –us-Sunnah Baghawi aliyefariki duniya mwaka wa 510 Hijiriya, ameandika hivi katika tafsiri yake iitwayo Ma’lam –al- Tanzil: Allah ameumaliziya mnyororo wa Manabii kwake (Muhammad), hivyo, Yeye ni Nabii wa mwisho... Ibn Abbas anasisitiza kwamba (katika aya husika), Allah amekata hukumu kuwa hakuna Nabii atakayekuja baada ya Muhammad (juzuu 3 uk.158). Zamakhshri aliyeishi miyaka ya 467-538 Hijiriya, ameandika hivi katika tafsiri yake inayoitwa Kashshaaf: “Iwapo unahoji inakuwaje Muhammad awe mwisho wa Manabii wakati Nabii Issa (Yesu) atatokeya tena mwishoni mwa duniya? Nitajibu kwamba mwisho wa unabii wa Muhammad maana yake hakuna mtu atakayepewa unabii baada yake. Nabii Issa yeye ni miyongoni mwa wale waliokwishapewa Unabii kabla ya Muhammad, isitoshe Nabii Issa atatokeya kama mfuwasi wa Muhamamd na ataswali kwa kuelekeza uso wake kibla akiwa miyongoni mwa Umma wa Muhammad” ( Juzuu ya 2 uk.215).

 

Qazi’ lyad aliyefariki duniya mwaka 544 Hijiriya, ameandika hivi; Yule anayezusha dai la unabii kwamba mtu anaweza kupata tena ofisi ya unabii au anaweza kupata hadhi ya Nabii kutokana na utakatifu wa nafsi kama inavyodaiwa na wanafalsafa na masufi; na vilevile hata mtu asiyedai kuwa Nabii lakini anatangaza kuwa amepokeya wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wote hawa ni murtadi wanaokanusha unabii wa Muhammad kwani Muhammad (s.a.w) amefikisha ujumbe wa Allah kwetu kuwa yeye akiwa wa mwisho,ameifunga kabisa ofisi ya Nabii na kwamba yeye ametumwa kama Nabii na Mtume kwa walimwengu wote. Ni maafikiyano ya ummah mzima wa Kiislamu kwamba maneno haya ya Mtume mtukufu yako wazi kabisa na kwa ufasaha yanaeleza ukweli kuwa hayaruhusu tafsiri nyingine yoyote wala sahihisho katika maana yake. Hivyo hapana shaka kuwa vikundi vinavyotowa tafsiri tofauti vimejitowa katika wigo wa Uislamu siyo tu kwa mtazamo wa shura ya umma bali kwa msingi wa maneno haya yaliyosambazwa kwa usahihi mkubwa (Shifa, juzuu ya 2 uk.270-271). Alamaa Shahrastani aliyefariki duniya mwaka 548, katika kitabu chake mashuhuri Al milal wan Nahal ameandika hivi; “Na kadhalika yule asemaye kuwa atakuja Mtume baada ya Muhammad (s.a.w) hakuna hukumu ila moja tu kuwa mtu huyo ni kafiri (Taz. Juzuu 3 uk 249) Imam Razi aliyeishi miyaka ya 543-606 Hijiriya, katika tafsiri yake iitwayo Tafsir al Kabir , akifafanuwa maana ya Khatam- un –Nabiyyin anasema: “Katika muktadha huu istilahi Khatam-un-Nabiyyin imetumika kwa maana kuwa nabii ambaye kipindi chake si cha mwisho anaweza kuwacha baadhi ya hukumu na amri zikiwa hazijakamilika au hazijapambanuliwa hali inayotowa nafasi ya kuja tena Nabii baada yake ili akamilishe kazi hiyo. Lakini Nabii ambaye hatakuwa na Nabii wa kumfuatiya anakuwa na kazi zaidi ya kukidhi haja zote na kutowa miyongozo iliyowazi kwa wafuasi wake kama vile baba anayejuwa kuwa baada yake hakutakuwa na mlezi wala mhisani wa kumleea mwanawe” (Taz. juzuu ya 6 uk.581) Alamaa Baidawi aliyefariki duniya mwaka 685 Hijiriya, katika tafsiri yake, Anwar-ul-Tanzil, ameandika hivi; “kwa maneno mengine, yeye Muhammad (s.a.w) ni mwisho wa Manabii. Ni kwake yeye ule mlolongo wa Mitume umeishiya. Au tuseme ni Mtume ambaye kuja kwake kumefunga ofisi ya Unabii. Kuja tena kwa nabii Isa (a.s) baada ya Mtume (s.a.w) hakuna mpingano na dhana ya mwisho wa unabii baada ya utume wa Muhammad (s.a.w). Kwa sababu Nabii Isa (as) atakuja kufuata shariya ya Muhammad” (Taz. Juzuu ya 4 uk.164) Alamaa Hafizu-ud-Din Al- Ansafi aliyefariki duniya mwaka 710 Hijiriya, katika tafsiri yake, Madark-ut-Tanzil, ameandika hivi: “Na yeye Muhammad ndiye ambaye ameumaliziya mlolongo wa Mitume.. Kwa maneno mengine, yeye ni mwisho wa Manabii wote. Mwenyezi Mungu hatateuwa tena Nabii baada yake. Kuhusu Nabii Isa (a.s) inaweza kusemwa kuwa yeye ni miongoni mwa wale walioteuliwa kuwa Manabii kabla ya zama za Muhammad (s.a.w). Na pale Nabii Isa atakapokuja tena, atakuwa mfuwasi wa shariyah ya Muhammad (s.a.w) na atakuwa miyongoni mwa waumini wa kawaida”.(uk.471) Alamaa Alau-din Bughdadi aliyefariki duniya mwaka 725 Hijiriya, katika tafsiri yake iitwayo Khazin, ameandika hivi: “Wa khatam–un-Nabiyyin”, kwa maneno mengine, Mwenyezi Mungu amekamilisha utume kwa Muhammad. Baada yake hadi mwisho wa duniya, hakuna tena unabii wala hakuna mshirika wake katika unabii..”Wa KanAllahu Bikulli Shaiin Alima” Mwenyezi Mungu anajuwa kuwa hakuna Nabii atakayekuja baada yake. (uk 471-472). Alamaa Ibn Kathir aliyefariki duniya mwaka 774Hijiriya, katika tafsiri yake mashuhuri sana iitwayo Tafsir Ibn Kathir , ameandika hivi: “Ndiyo kusema aya hii ni uthibitisho wa wazi wa ukweli kuwa “hakuna Nabii atakayekuja baada ya Muhammad (s.a.w) na inaposemwa kwamba hakuna Nabii atakayekuja baada yake basi ndio hitimisho la jumla kuwa hakuna Mtume atakayemfuatiya kwani ofisi ya utume ina mvumo zaidi ya ofisi ya Nabii. Kila Mtume ni Nabii lakini si Manabii wote ni Mitume. Yeyote anayezusha dai la Unabii baada ya Muhammad ni Muwongo, Mvurugaji, Mzushi, mtovu wa maadili, na mpotoshaji hata akiwa na mauzauza au mazingaombwe. Yeyote yule atakayezusha dai hilo anaingiya katika kundi hili (Taz. Juzuu ya 3 uk.493-494). Allamaa Jalal-Ud-Din Suyut aliyefariki duniya mwaka 911Hijiriya, katika Tafsiri yake iitwayo Jalalain, ameandika hivi: ”MwenyeziMungu ajuwa fika ukweli kuwa hakuna Nabii atakayekuja baada ya Muhammad na pale Isa (a.s) atakapokuja tena duniyani ataishi kwa kufuwata shariya ya Muhammad” (uk.768) Alamaa Ibn Nujaim aliyefariki duniya mwaka 970 Hijiriya, katika kitabu chake mashuhuri cha kanuni za fiqh kiitwacho Al Ashbah wan-Nazair, Kitab -us-Siyyar: bab: al Radda, ameandika hivi: “Mtu asiyemuitakidi Muhammad kama Mtume wa mwisho wa Allaha si Muislamu kwani kuamini Unabii wa Muhamad kuwa ni wa mwisho ni moja kati ya vipengele vya msingi vya imani ambavyo Muislamu lazima avielewe na kuviamini (uk 179). Mulla Ali Qari aliyefariki duniya mwaka 1016 Hijiriya , katika tafsiri yake, Fiqh Akbar ameandika hivi; “Kuzusha dai la Unabii baada ya kipindi cha Mtume wetu Muhammad (s.a.w) ni ukafiri mkubwa , hili ni tamko la pamoja la ummah wa Kiislamu (uk. 202). Sheikh Ismail Haq aliyefariki duniya mwaka 1137Hijiriya akisherehesha aya husika ameandika hivi katika tafsiri yake Ruh-ul -Bayan.” Asim hulisoma neno Khatam kwa fat-ha juu ya herufi te ambayo maana yake ni kifaa cha kupigiya muhuri na kufunga kama vile “Printer” mashine ya kupigiya chapa. Maana ya neno hilo ni kwamba, Mtume mtukufu alikuwa mwisho wa Manabii na MwenyeziMungu ameifunga kabisa ofisi ya unabii kupitiya utume wake. Katika lugha ya Kiajemi (kipersia) maana kama hiyo inaelezwa kwa istilahi “Mohar Paighambran”, Komeo au kifungio cha Manabii, yaani kuja kwa Muhammad kumefunga mlango wa unabii na hivyo ule mlolongo wa Manabii umeishiya kwake. Wasomaji wengine wanalitamka neno Khatim kwa qasra chini ya neno te ambayo maana yake ni kusema kuwa Muhammad alikuwa Mtume aliyefunga milango ya unabii. Katika lugha ya kiajemi (kipersia) maana hiyo inaelezwa kwa istilahi Mohar konindai Paighambran komeo la Manabii, kwa hiyo, kwa namna zote mbili,neno khatam linabeba maana ile ile moja.. Kwa hiyo Maulamaa wa Umati Muhammad watarithi tu hadhi ya utakatifu wa kiroho kutoka kwake lakini urithi wa hadhi ya unabii haupo tena, kwani Muhammad amefunga kabisa ofisi ya unabii kwa zama zote zijazo... Kuja tena kwa nabii Isa (a.s) baada ya Muhammad hakupingani na mwisho wa unabii kwa Muhammad. Maneno Khatam-un-Nabiyyin yanabainisha wazi kuwa hakuna mtu mwingine atakayeteuliwa kuwa Nabii baada ya Muhammad (s.a.w). Nabii Isa (a.s) alikwishateuliwa kuwa Nabii kabla ya Muhammad na yeye Isa atakuja kuwa mfuwasi wa shariya ya Muhammad (s.a.w). Nabii Isa (a.s) atasali swala kwa kuelekeza uso upande wa Qibla alikoelekeya Muhammad (s.a.w). Nabii Isa (as) atakuwa miyongoni mwa Waumini Waislamu. Yeye hatapokeya wahyi wowote kutoka kwa MwenyeziMungu wala hatoleta sheriya mpya; ataishi kama mfuwasi wa Muhammad (s.a.w). Dhehebu la suni (Ahl-Sunnat wal Jama’a (Suni) wanaitakidi kuwa hakuna Nabii atakayekuja baada ya Mtume mtukufu (s.a.w) kwa sababu MwenyeziMungu amesema “Wa-lakin rasul Allahi wa Khatama-un-Nabiyyin”..., na Mtume amesema: La Nabiya Ba’d (hakutakuwa na Nabii baada yangu). Hivyo , yeyote anayesema kuwa kuna Nabii atakayemfuatiya Muhammad (s.a.w) atakuwa Murtad kwa sababu amekanusha kipengele cha msingi cha imani. Halikadhalika yeyote anayeutiliya shaka mwisho wa unabii wa Muhammad naye piya atatangazwa kuwa ni kafiri, kwani maelezo yote hayo yamepambanua haki na batili na dai lolote la Utume baada ya Muhammad ni batili kabisa” Katika Fatawa-i-Alamgiri iliyokusanywa na wanazuwoni wa Barahindi kwa agizo la Aurangzed Alamgir, katika karne ya 12 Hijiriya, imeandikwa hivi: “Mtu asiyemuitakidi Muhammad kama Mtume wa mwisho wa MwenyeziMungu, si Muislamu na, na kama mtu huyo anadai kuwa yeye ni mtume au nabii, atatangazwa kuwa ni murtad”. (Juz. 2, uk.263). Allama Shoukani aliyefariki duniya mwaka 1255Hijiriya, katika tafsiri yake, Fath-ul-Qadiir ameandika hivi: Watu wengi wamelisoma neno Khatam kwa Qasra chini ya te lakini “Asim hulisoma neno hilo hilo kwa fat-ha juu ya te. Kisomo cha kwanza kina maana kuwa Muhammad alikamilisha mlolongo wa Mitume yaani kwa maneno mengine Mtume Mtukufu alikuja mwishoni kabisa mwa Mitume wote. Kisomo cha pili kina maana kuwa Mtume mtukufu alikuwa komeo ambalo kwalo ofisi ya unabii ilifungwa kabisa; na kuja kwake kukaleta rehema kwa kundi la Mitume wa Allah. Allama Alusi aliyefariki duniya 1270Hijiriya, katika tafsiri yake, Ruh-ul-Ma’ani, ameandika; neno nabii ni la jumla, lakini neno “Mtume” lina uzito mahususi. Ndiyo kusema pale Nabii anapoitwa “komeo la Manabii basi ni lazima piya awe “komeo la mitume”. Maana ya ile nafasi ya Mtume mtukufu ya kuwa ‘Mwisho wa Manabii na Mitume wote ni kwamba kwa kwa kupandishwa kwake katika hadhi ya Unabii katika duniya hii, basi hadhi hiyo ndiyo basi imekoma na hakuna mtu anayeweza kuifikiya hadhi hiyo hivi leo.” (Juz. 22 uk.32). “Yeyote anayejidai kupokeya wahai kutoka kutoka kwa Allah kama nabii baada ya kuondoka Muhammad, atatangazwa kuwa ni kafiri. Hakuna tofauti ya rai miongoni mwa Wanazuoni juu ya jambo hili.”.(Juz. 22, uk. 38). Uthibitisho wa Kitabu cha MwenyeziMungu kuwa Muhammad ni Mwisho wa Mitume uko wazi. Hadith zimelifafanuwa bayana hili na Umma umeafikiyana juu ya hili. Ndiyo kusema anayetowa dai la kupinga msimamo huu atatangazwa kuwa ni murtadi (Taz. Juz. 22, uk. 39).

Hizi ni fafanuzi za waja waongofu, Mafuqaha, Wanazuwoni wa Hadith na Mufasiruna wa kila nyanja ya Uislamu tokeya Bara Hindi hadi Morocco na Hispania (Andulus), na tokeya Uturuki hadi Yemen. Tumeonesha miyaka yao ya kuzaliwa na kufa katika kila tukiyo ili msomaji kwanza atambuwe kuwa orodha hii inajumuisha Wanazuoni mashuhuri wa kila karne ya historiya ta Uislamu iliyoanziya baina ya karne ya kwanza na ya kumi na tatu.

Tungeliweza hata kuongeza fafanuzi za Madaktari weledi wa Uislamu wa karne ya kumi na nne; lakini tumewaacha Maulamaa wa karne ya kumi na nne kwa makusudio maalum kwa sababu mtu fulani angeweza kusema kuwa labda Wanazuwoni hawa walikuwa wamefafanuwa maana ya Khatam-i-Nabuwat kama “komeo la Mitume” ili kukanusha dai la Mitume wapya wa zama hizi.

Hivyo, haiwezi kusemwa kuwa Maulamaa wa karne zilizopita walikuwa na chuki dhidi ya watu wa zama za leo wanaodai kuwa ni Mitume. Maandiko piya yanadhihirisha bila shaka yeyote kuwa tokeya karne ya kwanza hadi leo hii ulimwengu wa Waislamu, kwa ujumla, umelichukuliya neno Khatam-un-Nabiyyin kwa maana ya “Mwisho wa Mitume wote”.

Waislamu wa vipindi vyote wamekuwa na imani moja kuwa ofisi ya utume imefungwa baada ya kuja kwa Mtume mtukufu (s.a.w). Hapajawahi hata kidogo kuwa na tofauti ya rai miongoni mwa Waislamu kwamba mtu yeyote anayediriki kujinadiya utume na wale wanaoamini dai la utume, wote hao wamejitowa nje ya wigo wa Uislamu.

Sasa ni juu ya watu wote wenye akili timamu kukata hukumu kuwa kutokana na ushahidi wote huu mzito; maana ya wazi ya kamusi ya kirai “Khatam-un-Nabiyyin”, tafsiri ya aya ya Qur’an kwa mawanda yake sahihi, ufafanuzi wa Mtume mwenyewe, muwafaka juu ya utume kuishiya kwa Muhammad uliofikiwa na Shura ya Umma mzima wa Waislamu ulimwenguni tokea Maswahaba wa Mtume mtukufu hadi waislamu wa leo.

Ni mwanya gani tena uliobaki wa kupachikiya tafsiri nyingine na ni hoja gani wanayoweza kuitowa kwa ajili ya kumfunguliya mlango wa utume mzushi yeyote yule.

Isitoshe watu hawa wanawezaje kutambuliwa kama Waislamu kwa sababu siyo tu wametowa rai yao kwa ajili ya kufunguwa mlango wa utume bali piya wamempandisha mtu katika daraja la Mitume wa Mungu na wamekuwa wafuwasi wa Muwovu huyo? Kwa mnasaba huu mambo haya matatu ni ni muhimu kuyazingatiya.

Je Mungu ni Adui wa Imani yetu?

Kwanza kabisa, Utume ni jambo nyeti. Kwa mujibu wa Mtume mtukufu utume ni kipengele cha msingi cha Imani, na kwamba yule anayeamini utume ndiyo muumini na yule asiyeamini ni Kafiri. Kama mtu hamuwamini Mtume, basi huyo ni Murtadi. Vile vile kama ataamini dai la mtu anayedai utume, mtu huyu huwa kafiri.

Katika jambo hilo nyeti na muhimu Mungu Muweza wa yote, kwa hakika, hawezi hata kidogo kudhaniwa kuwa ameteleza. Kama kumgelikuwa na Mtume baada ya kipindi cha Muhammad MwenyeziMungu angeliutangaza bayana uwezekano wa kuja nabii mwingine.

Katu Mtume wa Allah asingelitawafu bila kuwabashiriya watu wake kuwa Mitume wengine wangekujs baada yake na kwamba wafuwasi wake lazima wawaamini Mitume hao wa baadae.

Je Mungu na Utume Wake walikuwa na niya yeyote ya kudhoofisha imani yetu kwa kutuficha uwezekano wa kufunguka mlango wa unabii na kuja nabii mwingine baada ya kipindi cha Muhammad na hivyo kutuwacha sisi katika utatanishi kwamba kama tusipoamini unabii wa nabii mpya basi tutatoka katika Uislamu?

Zaidi ya hivyo, piya tungeliwekwa gizani na Mungu na Mtume Wake juu ya jambo hili, lakini kinyume chake walitowa maelezo na uthibitisho ambao Umma, kwa miyaka elfu moja miya tatu (sasa miyanne) iliyopita haujayapa maana nyingine na hadi leo bado una mtazamo ule ule kuwa hakuna nabii atakayekuja baada ya Muhammad. Je Mungu na Mtume Wake kweli wangeliweza kuicheza shere imani yetu?

Jaaliya kwa muda tu mlango wa ofisi ya unabii unafunguliwa na Mtume mwingine anajitokeza, sisi, bila shaka, tutamkataa. Kwa kukataa huku, Mungu anaweza kutuhukumu siku ya hukumu; lakini nasi tutawasilisha mbele yake rekodi yote ya maneno na hukumu zake.

Ushahidi huu (SubhanAllah) utathibitisha kuwa Kitabu cha Allah na Sunna ya Mtume Wake zilituchuza na hivyo kutomwamini Mtume mpya na kwa hivyo ametuhukumu kwa ukafiri. Hatuna wasiwasi kuwa baada ya kuitafakari rekodi hii Mwenyezi Mungu ataona yaswihi kutuadhibu kwa kufuru dhidi ya Mtume mpya.

Lakini kama mlango wa utume unafungwa ambapo hakuna Mtume atakayekuja baada ya Muhammad, lakini pamoja na ukweli huu bado mtu analisadiki dai la Mtume mpya, mtu huyo afikirie vizuri kweli kweli ni rekodi gani atakayoiwasilisha mbele ya Mungu katika kujiteteya kwake ili kuepukana na adhabu ya kufuru na kupata nusra?

Mtu huyo anapaswa kupitiya rekodi yake ya kujiteteya kabla ya kufikishwa mbele ya mahakama kuu ya MwenyeziMungu. Ailinganishe rekodi yake na ile tuliyoiwasilisha sisi na kisha ajihukumu mwenyewe iwapo rekodi anayoitegemeya kwa utetezi wake inaswihi kwa mtu mwenye akili timamu na je anaweza kusimama mahakamani kuhimili hatari ya kukabiliyana na shitaka la kufuru na kuadhibiwa kwa shitaka hilo kwa ile aina ya utetezi alionao mikononi mwake?”

Je twahitaji Mtume mpya hivi sasa?

Nukta ya pili, inayohitaji mazingatiyo ni kwamba unabii sio daraja analoweza kupata mtu yeyote anayejiona anastahili kulipata kwa kujitupa kwake katika sala na mambo ya UchaMungu. Wala si kitu kilicho sawa na zawadi au tuzo ya utumishi bora. Unabii ni madaraka ambapo Allah humteuwa mtu fulani katika madaraka hayo kutimiza hitajiyo fulani.

MwenyeziMungu hatumi Mitume kwa mfuwatano wa harakaharaka iwapo hakuna hitajio au pale ambapo hitajio limetimizwa. Tunapoirejeleya Qur’an ili kuona masharti ambayo kwayo Mitume wameletwa ulimwenguni, tunaona kuwa kuna masharti manne ambayo kwao Manabii walitumwa duniyani:

Mosi, kulikuwa na haja ya Mtume kupelekwa katika Taifa fulani ambako hapo kabla hakuna mtume aliyepata kupelekwa na ujumbe ulioletwa na Mtume wa Taifa jingine usingeweza kuwafikiya watu wa Taifa hilo.

Pili, kulikuwa na haja ya kumteuwa Mtume kwa sababu ujumbe wa Mtume wa awali ulikuwa umesahauliwa na watu, au mafundisho ya Mitume waliopita yamevurugwa na hivyo ikawa vigumu kufuwata ujumbe ulioletwa na Mtume husika.

Tatu, watu hawakupokeya sharia kamili ya Allah kupitiya Mtume aliyetanguliya. Hivyo Mitume waliofuwata walitumwa ili kutimiza jukumu la kukamilisha dini ya Allah

Nne, kulikuwa na haja ya Mtume wa pili kushirikiana na Mtume wa kwanza kutimiza jukumu la ofisi moja

Ni dhahiri kuwa hakuna hitajio lolote kati ya mahitajiyo hayo ambalo limesaliya baada ya kipindi cha Mtume Muhammad.

Qur’an tukufu inasema kuwa Nabii Muhammad katumwa kama mjumbe wa kufikisha mawaidha kwa Walimwengu wote. Historiya ya utamaduni ulimwenguni inathibitisha ukweli kuwa kabla ya kipindi cha Mtume Muhammad (saw), masharti hayo mara kwa mara yalijuzu ulimwenguni kwa ajili ya kusambaza ujumbe katika Mataifa yote.

Lakini kwa sasa Mataifa hayahitaji tena Mitume tofauti baada ya kipindi cha Mtume Muhammad. Qur’an tukufu na Hadith na sira ya Muhammad vinathibitisha ukweli kuwa ujumbe wa MwenyeziMungu ulioletwa ulimwenguni na Mtume mtukufu uko vilevile katika muundo wake halisi na asiliya. Ujumbe wa Mtume haujakumbwa na heka heka za uharibifu na upotoshaji.

Hakuna hata neno moja lililoongezwa au kufutwa katika Qur’an tukufu, kitabu alichokileta Mtume duniyani kutoka kwa MwenyeziMungu, wala hakuna yoyote awezaye kutiya nyongeza au kupunguza chochote kutoka humo hadi siku ya kufufuliwa.

Ujumbe ambao Mtume mtukufu ameufikisha kwa maneno na vitendo umesambazwa kwetu katika muundo wake uleule kamili, halisi na asiliya kiasi ambacho tunahisi kama vile tunaishi katika mazingira na zama za Mtume Mtukufu.

Kwa hiyo sharti la pili la kuletwa Mitume ulimwenguni limetimizwa.

Tatu, Qur’an inathibitisha waziwazi kuwa MwenyeziMungu amekamilisha utume kupitiya utume wa Nabii Muhammad. Ndiyo kusema hakuna tena nafasi kwa Mtume mpya kuja kukamilisha kazi ya Mungu.

Kuhusiyana na sharti la nne, iwapo mwenza kweli angehitajika, basi angeteuliwa katika zama za Mtume Muhammad ili kushirikiyana jukumu zito la kipindi chake. Kwa vile hapakuwa na Mwenza aliyeteuliwa sharti hili nalo piya limetimizwa.

Hivyo basi tuangaliye huku na kule kupata sharti la tano ambalo kwalo Mtume mpya labda anaweza kuhitajika baada ya Muhammad. Ikiwa mtu anatowa hoja kuwa watu wametumbukiya katika uovu, hivyo kuna haja ya kuja Mtume mpya kuwarekebisha watu waovu, sisi tutamuuliza hivi;

lini Mtume aliwahi kuja kuanzisha mageuzi tu ambapo tunahitaji Mtume mwingine wa kutekeleza kazi ya mageuzi? Mtume huteuliwa ili awe mpokeaji wa wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wahyi wa Mwenyezi Mungu hushushwa kwa lengo la kusambaza ujumbe mpya au kusahihisha makosa ambayo yametumbukizwa katika dini baada ya ujumbe wa awali.

Kwa vile Qur’an na Sunna ya Mtume vimehifadhiwa katika muundo wake uleule wa asili na timilifu na kwa vile kazi ya Mungu imekamilishwa na Muhammadi basi hitajio lolote liwalo la kusambaza wahyi wa Mungu hivi sasa limetimizwa ambapo hitajiyo lililopo ni lile la Mujitahidi wa kuondosha maovu ya wanadamu, lakini hakuna nafasi kwa Mitume wengine.

Part 2..Finality of Prophethood by Maudodi

تاريخ الاضافة: 26-11-2009
طباعة